Kizazi Kipya Wanapozifikisha Taka Ngumu Mahakamani
Locations
Themes
Projects
Third Alternative
Kile ambacho vijiji viwili Mkoani Kagera vinaifundisha Tanzania kuhusu usimamizi wa taka ngumu
Hebu fikiria mchana mmoja wa Jumanne pale Kabingo. Shule zimefungwa kwa siku hiyo. Kundi la watoto, wengine wadogo kiasi kwamba gunia wanalobeba ni kubwa kuliko wao, wanatembea taratibu kwenye njia iliyo nyuma ya nyumba. Wanainama na kuokota chupa ya maji iliyobonyezwa, pakiti ya juisi, kifungashio kilichochanika. Mmoja wao anahesabu. Kufikia jioni, magunia yamejaa, na njia inaonekana kama ilivyokuwa kabla plastiki haijafika kijijini.
Je, itakuwaje kama moja ya mawazo bora zaidi ya Tanzania kuhusu kushughulikia taka halikutoka maabara wala ofisini, bali kutoka kijijini ambako watoto waliamua kuifikisha plastiki mahakamani?
Katika vijiji vya Kabingo na Kitobo, Wilaya ya Missenyi, Mkoa wa Kagera, vijana na jamii zao wamefanya hivyo hasa. Wanaiita Mahakama ya Taka Ngumu. Baadhi ya watoto huwa mawakili, wakiwasilisha ushahidi na kujenga hoja zao, huku wengine wakiwa majaji wanaoamua hatima ya vitu vilivyotupwa. Ushahidi huletwa kwenye magunia: huchambuliwa kwa mkono na kupimwa kwa kilo. Hukumu ya kwanza ya mahakama hii ni rahisi: jamii za vijijini zina tatizo halisi la taka ngumu, na kusubiri huduma ya ukusanyaji ya mtindo wa mjini hakutalifanya tatizo hili kutoweka.
Makala hii inaeleza kile ambacho watoto wamegundua, mahali ambapo mipango ya kitaifa inaviacha vijiji nyuma, na kile kinachopaswa kufanyika sasa.
Tatizo la Dunia Linalofika Hadi Kijijini

Dunia inazalisha taka zaidi kila mwaka. Benki ya Dunia inakadiria kwamba mwaka 2022 dunia ilizalisha tani bilioni 2.56 za taka za majumbani na mijini. Hali isipobadilika, kiasi hicho kinaweza kufikia tani bilioni 3.86 kwa mwaka ifikapo mwaka 2050.
Lakini swali lenye uzito zaidi: Nini hutokea bidhaa zilizofungashwa zinapofika kijijini ambako hakuna anayekusanya, kuchambua wala kuondoa mabaki? Yeyote aliyewahi kupita kwenye kituo cha biashara cha kijijini siku ya gulio anajua jibu. Taka huishia kwenye udongo na maji. Huziba mitaro na kuongeza mafuriko. Zinapotupwa ovyo au kuchomwa, huchafua hewa ambayo familia huivuta.
Vijiji Vinasahaulika
Tanzania tayari inapata changamoto kubwa katika kushughulikia taka zake. Utafiti wa mwaka 2021 wa Centre for Science and Environment (CSE) ulikadiria kwamba nchi inazalisha tani milioni 12 hadi 17 za taka kwa mwaka. Ni karibu nusu tu inayokusanywa. Karibu theluthi moja ya taka zote hufukiwa ardhini, na karibu sehemu moja ya sita hutupwa popote penye nafasi. Ni asilimia 5 hadi 10 tu zinazochakatwa na kutumika tena, na zaidi ya asilimia 90 hazitupwi kwa njia salama.
Kuna tatizo jingine pia: tunaufahamu mdogo kuhusu taka za vijijini. Utafiti huo huo uligundua kwamba tafiti nyingi nchini Tanzania zilifanyika Dar es Salaam, na matokeo hayo ya jiji mara nyingi yalitumika kuelezea nchi nzima. Kwa hiyo, vijiji vinapata msaada mdogo, na taka zake hazihesabiwi ipasavyo.
Kisheria, jambo hili liko wazi. Sheria ya Usimamizi wa Mazingira inazipa halmashauri jukumu la kukusanya taka mijini na vijijini, kama tathmini ya CSE inavyoeleza. Lakini vijiji vingi bado havina mapipa, vituo vya kukusanyia, usafiri, mahali pa kuchambulia taka, wanunuzi wa vitu vinavyoweza kuchakatwa na kutumiwa upya wala mahali salama pa kutupa kinachobaki. Hili si tatizo la mjini lililosambaa hadi vijijini. Ni tatizo la kijiji.
Kumbuka kitu cha mwisho ulichonunua kwenye genge au duka la mjasiriamali kijijini: soda, pakiti ya mafuta ya kupikia, biskuti. Kilifika kwa lori, pikipiki au baiskeli. Lakini hakuna anayerudi kuchukua pakiti tupu. Bidhaa inafika kijijini. Uwajibikaji kwa kifungashio chake haufiki. Ripoti ya CSE inasisitiza jambo hilo hilo: vifungashio vidogo ni rahisi kununua na vinapendwa, lakini ni vigumu kuvikusanya na haviwezi kurejelezwa, hivyo kampuni zinazoviuza zinapaswa kusaidia kuvirudisha.
Hata mjini, suala hili si la tabia za watu peke yake. Watafiti walipozungumza na wakazi 102 wa Manzese na Sinza jijini Dar es Salaam, sababu kubwa waliyoitaja ya kurundikana kwa taka ilikuwa gharama ya ukusanyaji. Wengi walisema ada ya kila mwezi ya shilingi 500 hadi 1,000 ilikuwa kubwa mno kwa kaya zao. Wengine walitaja ukosefu wa maeneo ya kutupia taka na sheria ndogo zisizosimamiwa. Ni takriban kaya moja kati ya kumi tu iliyokuwa ikitumia pipa la taka. Kama familia katika jiji kubwa kuliko yote nchini zinahangaika hivi, fikiria kijiji ambacho gari la taka lililo karibu liko umbali wa masaa kadhaa. Kuwaelimisha watu kuwa makini na taka husaidia, lakini haitoshi. Vijiji vinahitaji huduma inayofanya kazi, na wafanyabiashara, warejelezaji na halmashauri lazima wasaidie kuijenga.
Mipango ya Kitaifa Bado Inaangalia Mijini
Pengo hili si jipya. Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Taka Ngumu wa mwaka 2018 unaanza kwa kueleza kwamba taka ngumu za mijini ni tatizo kubwa la kimazingira. Unasema unalenga usimamizi mzuri wa taka “katika vituo vya mijini na vijijini”, lakini baada ya hapo unagusia maeneo ya vijijini kwa kupita tu, na malengo yake ya awali yaliwekwa kwa ajili ya “maeneo muhimu ya mijini”.
Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV), ulioanza Mwezi Julai 2026 hadi Juni 2031, unafuata njia hiyo hiyo. Unakiri kwamba nchi haisimamii taka zake vizuri, lakini unapoweka malengo yanayopimika, unaangalia zaidi miji na majiji.
Lengo lake kuu kuhusu taka ni kukusanya taka katika asilimia 60 ya maeneo ya mijini ifikapo Juni 2031. Hatua zilizo chini ya lengo hilo pia zinahusu mijini: malori zaidi, mapipa na vituo vya kukusanyia kwa maeneo ya mijini; mitambo mipya ya kuchakata na kurejeleza taka katika miji mikubwa; ubia na kampuni binafsi kujenga mitambo mikubwa ya urejelezaji; na kupunguza taka zisizokusanywa mijini kwa asilimia 30. Plastiki zinatajwa, lakini hasa kama uchafuzi baharini, maziwani na mitoni.
Vijiji vimeachwa nje ya malengo haya. Jambo hili linashangaza kwa sababu mpango huo huo unaweka malengo tofauti ya vijijini kwa maji safi na vyoo. Hakuna lengo linalolingana na hilo kwa ukusanyaji au utupaji salama wa taka vijijini. Kitu pekee ambacho huenda kikafika vijijini ni kampeni ya kitaifa inayowaelimisha watu jinsi ya kutupa taka kwa usalama, na kampeni peke yake haiwezi kukusanya hata mfuko mmoja.
Kisichohesabiwa mara nyingi hakipati fedha. Kama vijiji havimo kwenye malengo ya mpango, kuna uwezekano mkubwa havitakuwemo kwenye bajeti wala taarifa za halmashauri. Mipango ya utekelezaji ya kila mwaka inaweza kurekebisha hili kwa kuongeza lengo la ukusanyaji taka vijijini, kupima aina na kiasi cha taka zinazozalishwa vijijini, na kuweka lengo la kupunguza uchomaji na utupaji ovyo.
Kile Ambacho Mahakama ya Taka Ngumu Imegundua
Vijiji vya Kabingo na Kitobo vilianza na kile walichoweza kukiona: chupa za plastiki, vifungashio vya vyakula na taka nyingine za kila siku zinazozunguka nyumba, njia na maeneo ya umma. Swali lao lilikuwa rahisi: kijiji kinawezaje kushughulikia taka zake chenyewe pale ambapo hakuna huduma rasmi? Jibu la mahakama ni mchakato wa hatua kwa hatua: kukusanya, kupima, kuchambua, kusafirisha, kutumia tena au kuuza kinachoweza kuokolewa, na kutupa kwa usalama kinachobaki.
Katika Kijiji cha Kabingo, mzunguko wa kwanza wa ukusanyaji ulipata kilo 107. Mzunguko wa pili ulipata kilo 133: kilo 43 za chupa za plastiki na kilo 90 za taka nyingine. Hiyo ni kilo 240 kwa mizunguko miwili, karibu sawa na uzito wa watu wazima watatu, iliyookotwa kwa mikono ya watoto. Katika Kijiji cha Kitobo, takriban kilo 300 zilikusanywa, ingawa hiyo ni makadirio kwa sababu hapakuwa na mizani ya kupimia. Takwimu hizi zinaonyesha tu kilichokusanywa, si taka zote zinazozalishwa na vijiji hivyo.
Taka huletwa kwenye eneo la kukusanyia la mahakama, huchambuliwa, kisha husafirishwa kwa pikipiki hadi mahali zinapotupwa. Uchambuzi ni muhimu. Kwa mujibu wa tathmini hiyo hiyo, zaidi ya asilimia 70 ya taka za mijini nchini Tanzania ni mabaki ya vyakula na mimea yanayoweza kuoza na kugeuka mboji. Mchanganyiko wa Kabingo unaweza kuwa tofauti, ndiyo maana kupima na kuchambua taka hapa hapa kijijini kuna manufaa makubwa. Kunaonyesha kipi kinaweza kugeuzwa mboji, kipi kinaweza kuuzwa, kipi kinaweza kurudishwa kwa kampuni zilizokitengeneza na kipi lazima kitupwe kwa usalama.
Kila aina ya taka inahitaji mtu wa kuipokea: kaya kwa ajili ya mboji, wanunuzi na warejelezaji kwa plastiki, karatasi, kioo na chuma safi, na kampuni kurudisha vifungashio vyao wenyewe. Bila watu hawa, kuchambua taka kunazalisha tu mirundo iliyopangwa vizuri zaidi.
Kwa sasa, taka zisizoweza kutumika tena wala kurejelezwa huchomwa kwenye kichomeo cha taka katika zahanati ya kijiji. Huu ni mwanzo wa vitendo wakati jamii zikiendelea kujenga mfumo kamili zaidi wa usimamizi wa taka. Kadiri mpango huu unavyokua, hatua inayofuata itakuwa kutathmini kama kichomeo hicho kinafaa kwa taka zinazoshughulikiwa, na kutafuta njia salama zaidi za kudumu za kuchakata taka. Kila suluhisho linaloongozwa na jamii huanzia mahali fulani. Vijiji vya Kabingo na Kitobo, tayari vimefanikisha jambo muhimu: zimewaleta watu pamoja kukusanya, kuchambua, kupima na kujadili taka zao, na hivyo kuweka msingi wa huduma endelevu ya usimamizi wa taka kijijini.
Plastiki Inaharibu Mashamba ya Vijijini
Hebu mfikirie mkulima anayelima shamba lake kabla ya mvua, akikuta vipande vya mifuko na vifungashio vya zamani katika kila mstari. Katika vijiji vya wakulima kama Kabingo na Kitobo, plastiki isiyokusanywa mara nyingi huishia pale chakula kinapolimwa. Hufagiliwa bustanini, hutupwa pembeni mwa mashamba, huchanganyika na samadi na mboji, au hufukiwa ardhini. Kitaifa, tathmini ya CSE iligundua kwamba karibu theluthi moja ya taka zote hufukiwa badala ya kukusanywa, na kijijini “kufukiwa” mara nyingi humaanisha kufukiwa kwenye ardhi ya mtu.
Na kiasi chake kinaongezeka. Jijini Dar es Salaam, sehemu ya plastiki katika taka za majumbani ilipanda kutoka asilimia 16 mwaka 2012 hadi asilimia 22 mwaka 2014, kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu zilizotumika katika Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Taka Ngumu. Maduka ya vijijini yanauza bidhaa zile zile, katika vifungashio vile vile.
Plastiki haiozi. Inavunjika tu kuwa vipande vidogo zaidi, vingine vidogo mno kiasi cha kutoonekana kwa macho, na vinaweza kukaa udongoni kwa miaka mingi. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limeonya kuhusu plastiki inayojilimbikiza mashambani. Vipande hivi vinaweza kuzuia maji ya mvua kupenya ardhini na kuufanya udongo ukauke haraka, jambo linaloathiri mazao zaidi wakati wa kiangazi. Vinaweza kuufanya udongo kuwa mgumu, hivyo mbegu hushindwa kuota vizuri na mizizi hushindwa kukua. Vinaweza pia kuwadhuru minyoo na viumbe vidogo vya udongoni vinavyogeuza mimea iliyokufa kuwa chakula cha mazao mapya. Na plastiki inapoingia kwenye samadi na mboji, kile kilichopaswa kurutubisha udongo huishia kusambaza plastiki badala yake. Hata mkakati wa taifa unataja uchafuzi wa udongo kama moja ya hatari za kutupa taka ovyo.
Kuchoma plastiki hakutatui tatizo. Majivu na moshi huacha kemikali hatari zinazotua kwenye ardhi inayotumika kwa mazao na malisho. Mifuko ya plastiki iliyozagaa pia inaweza kuwaua ng’ombe na mbuzi ambao familia huwategemea.
Kwa familia za wakulima zinazoishi kwa kutegemea mavuno ya kila msimu, hili ni suala la chakula na kipato, si la mazingira peke yake. Mpango wa taifa wenyewe unasema utunzaji duni wa rutuba ya udongo unapunguza mavuno, na unalenga kupunguza ardhi iliyoharibika kutoka asilimia 16 hadi 14 ifikapo 2031. Kuzuia plastiki isiingie mashambani kunapaswa kuwa sehemu ya juhudi hizo. Kila kilo inayokusanywa na Mahakama ya Taka Ngumu ni kilo ambayo haitaishia kwenye mashamba yanayolisha kijiji.
Kidogo Kidogo Hujaza Kibaba
Kiasi kilichokusanywa hadi sasa ni kidogo, lakini kinaweza kukua. Tuseme kila kijiji kinakusanya kilo 100 kutoka kila kimoja cha vitongoji vyake vinne kila baada ya miezi miwili. Hiyo ni takriban tani 2.4 kwa mwaka kwa kila kijiji. Kama vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vingefanya hivyo, jumla ingefikia takriban tani 29,563, karibu kilo milioni 30, kila mwaka.
Huu ni mfano, si utabiri. Unatokana na makusanyo machache tu na unadhani kwamba kila kijiji kinashiriki mara kwa mara na kina usafiri pamoja na mahali salama pa kupeleka taka. Hata hivyo, unaonyesha mambo mawili. Juhudi ndogo za vijiji zinaweza kuleta tofauti kitaifa. Lakini watoto na vijiji hawawezi kulitatua tatizo hili peke yao.
Vijana Wanaongoza, Watu Wazima Watimize Wajibu Wao
Kitu chenye nguvu zaidi kuhusu Mahakama ya Taka Ngumu si eneo la kukusanyia. Ni ile dakika mtoto anaponyanyua chupa na kuuliza, “Hii inatakiwa kwenda wapi?” Vijana wanageuza tatizo ambalo kila mtu alikuwa ameacha kuliona kuwa ushahidi ambao watu wazima, viongozi na kampuni hawawezi kuupuuza.
Mradi huu unahusisha wanafunzi 77 wa shule za msingi na sekondari. Kundi moja lina wanafunzi 16, wavulana 7 na wasichana 9 wenye umri wa miaka 4 hadi 16. Kundi jingine lina wanafunzi 61, wavulana 37 na wasichana 24 wenye umri wa miaka 7 hadi 14. Ni sehemu ya Kizazi Z (Gen Z) na Kizazi Alpha (Gen Alpha), lakini kilicho muhimu zaidi ni wanachokifanya: kugeuza wanachojifunza kuhusu mazingira kuwa vitendo halisi. Baada ya shule, hujiunga na shughuli za usafi zilizopangwa na kuwasaidia wazazi, majirani na viongozi wa kijiji kuona kile ambacho jamii inatupa na mahali kinapopaswa kwenda.
Usalama na kujifunza vinatangulia kwanza. Kabla ya kushiriki, wanafunzi hufundishwa jinsi ya kutambua na kuepuka sindano, taka za hospitali, kemikali na vitu vingine hatari. Hawachomi taka wala kuzibeba kwa njia isiyo salama. Ushiriki wao ni shughuli ya kujifunza kuhusu mazingira inayosimamiwa, inayojenga uwajibikaji, ushirikiano na upendo kwa jamii yao. Ili kutambua na kusherehekea mchango wao, Third Alternative na mshirika wake, Kabingo Agro Social Enterprise, huwapa wanafunzi vifaa vya shule baada ya kila mzunguko wa ukusanyaji. Msaada huu unaimarisha masomo yao na hauhusiani na kiasi wala aina ya taka zilizokusanywa, hivyo watoto hawahamasishwi kamwe kukusanya taka zaidi au kujiweka hatarini.
Kinachopaswa Kufanyika Sasa
Mahakama ya Taka Ngumu ilianzia katika vijiji viwili, lakini inaibua swali kwa nchi nzima: kijiji kikishakusanya, kupima na kuchambua taka zake, nani anachukua jukumu kuanzia hapo?
Kijiji kinaweza kuandaa usafi na kuhesabu taka zake. Lakini hakiwezi, peke yake, kutengeneza soko la vitu vilivyorejelezwa, kuzilazimisha kampuni kurudisha vifungashio vyao, kulipia usafiri wa masafa marefu au kuidhinisha eneo salama la kutupia taka. Halmashauri za wilaya, warejelezaji, wazalishaji, shule, vituo vya afya na wafadhili kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake. Mshirika wetu, Kabingo Agro Social Enterprise, anaweza kusaidia kwa kuwaleta watu pamoja, kuratibu ukusanyaji na kukiunganisha kijiji na halmashauri na wafanyabiashara. Lakini hawezi kufanya kazi zao kwa niaba yao.
Hili linaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 (DIRA 2050), inayotoa wito wa kupunguza uchafuzi, kuboresha usimamizi wa taka na kutengeneza kipato kutokana na vitu ambavyo watu hutupa. FYDP IV, mpango unaoitekeleza dira hii katika miaka mitano ijayo, unapaswa kujumuisha vijiji katika malengo yake ya taka. Vijiji vya Kabingo na Kitobo vimeonyesha jinsi hilo linavyoweza kutekelezeka kwa vitendo.
Mafanikio yanapaswa kupimwa kwa zaidi ya kilo zilizokusanywa. Tunapaswa pia kuuliza: Je, taka zinachambuliwa kwa usalama? Je, kila aina inafika mahali sahihi? Huduma inagharimu kiasi gani, na nani analipa? Je, inaweza kuzalisha kipato? Je, plastiki kidogo inaishia mashambani? Je, taka kidogo zinachomwa au kutupwa ovyo?
Watoto wamewasilisha kesi yao. Wametembea njiani, wamejaza magunia na kuhesabu kila kilo. Vijiji vinahitaji zaidi ya ushauri kuhusu taka. Vinahitaji huduma inayounganisha juhudi za jamii na msaada kutoka serikalini, kwa kampuni na kwa warejelezaji. Third Alternative inazikaribisha halmashauri, wazalishaji, warejelezaji, shule na wafadhili kusaidia kuijenga. Mahakama iko kikaoni. Nani atajibu?
Locations
Themes
Projects